Murphy hakushangazwa sana na mandhari ya jumba la Debbie. Kwani alishaona mengi. Wakiendelea na maongezi yao sebuleni katika ghorofa ya kwanza, punde aliingia mama mmoja wa makamo; mfupi, mwembamba na kusimama mbele ya Murphy na Debbie. Kwa heshima kubwa Murphy alisimama – hali kadhalika Debbie, ambaye pia hakupoteza muda akawa ameanza utambulisho mara moja.
"Mama, kutana na … Peter Kennedy, kutoka Afrika. Ndiye yule niliyekusimulia jana kwamba nilionana naye. Na Peter kutana na mama yangu, Mama wa Kwanza wa Meksiko, Susan Patrocinio," Debbie alimtambulisha Murphy na Susan, wakati hapohapo Murphy akitoa tabasamu na kunyoosha mkono kushikana na mwanamke aliyekuwa na nguvu kuliko wote nchini Meksiko. Mama Susan alimvuta Murphy na kumkumbatia huku akimkaribisha na kumwambia ajisikie alikuwa nyumbani.
"Mwenzako ndiyo hivyo," alisema Mama Susan. "Kapatwa na matatizo wiki iliyopita na nadhani utamtia faraja. Anatupa wasiwasi," mama alimwomba Murphy.
"Ahsante, mama. Usiwe na hofu. Atapona," Murphy alikubali.
"Asante. Afrika unatokea wapi?"
"Natokea Zambia, mama. Lusaka."
"Lusaka ni mji mzuri sana! Nimefika Tanzania pia, Kenya na Zimbabwe. Nchi zenu ni nzuri sana."
"Sanasana tunajivunia amani na utulivu … na maliasili."
"Niliupenda sana Mlima Kilimanjaro, na Maporomoko ya Victoria. Karibu sana kwetu. Debbie … mbona hamna vinywaji?" mama aliisifu nchi ya Murphy na kumkumbusha mwanaye ukarimu.
"Nimeshamwagiza Jiminez, mama. Ataleta sasa hivi. Asante."
"Ahaa. Basi sawa. Nyie endeleeni; nitawaona baadaye," mama aliaga na kurudi kwake.
"Debbie, hufanani kabisa na mama yako?" Murphy aliuliza mara tu Mama Susan alipoondoka.
"Nafanana sana na baba … yuko Panama kwa ziara ya kikazi ya siku tatu."
"Nimempenda sana mama yako."
"Mama yangu hana matatizo kabisa na watu. Nampenda pia ..."
Salvatory Jiminez, Mpishi Mkuu wa Rais wa Meksiko, aliingia na sinia la dhahabu lililojaa vinywaji vya aina mbalimbali na udohoudoho. Alimimina vinywaji katika glasi halafu akamkaribisha Murphy na Debbie na kurudi jikoni.
Murphy na Debbie wakiendelea kunywa na kuongea, Debbie aliona haikuwa vyema kuendelea kukaa farashani. Alimwomba Murphy wahamie katika chumba cha kulala ili waendelee na maongezi yao kule wakati akijimwagia maji. Murphy hakulipinga hilo. Walichukua vinywaji vyao na kupanda juu mpaka ghorofa ya pili (mwisho) mpaka chumbani kwa Debbie. Murphy alikuwa hajawahi kuona chumba kizuri kama hicho pamoja na ujanja wake wote. Vitu vingi vilimvutia. Kilichomvutia zaidi hata hivyo ni picha tatu kubwa nyuma ya kitanda: wanawake wawili mwanamume mmoja, waliyoonekana kuwa wa muhimu sana kwa Debbie.
"Murphy, karibu chumbani kwangu," Debbie alimkaribisha Murphy huku akitabasamu, kiuchokozi.
"Ahsante; una chumba kizuri sana, Debbie. Gharama yake kiasi gani?"
"Milioni? Dola milioni?" Debbie alijibu, akibinua mdomo na mabega.
"Dola ya Marekani?"
"Dola ya Marekani."
John Murphy 'alibroo'. Chumba kilikuwa na jumla ya vyumba vinne, kitanda kikubwa cha hadhi ya kifalme, makochi ya kumeremeta, kompyuta, televisheni, zulia nene jipya jeupe, mapazia ya dhahabu ya Taffeta, kofia ya taa ya dhahabu ('chandelier', 'shandalia') ya Baccarat na vitu vingine vingi.
Debbie alimkaribisha Murphy katika kochi la karibu na kitanda na kumkaribisha tena kinywaji chake na njugu mawe. Waliweka vinywaji vyao katika meza ndogo ya kioo na kuendelea kuongea, Murphy akiwa amekaa katika kochi (dogo jeusi) na Debbie akiwa mbele yake katika stuli ndogo ya kioo – iliyokuwa na miguu myeusi – huku ameshikilia glasi ya mvinyo kwa mkono mmoja, na mwingine akiutumia kuchezea magoti Murphy, lakini kwa wasiwasi. Hakwenda kuoga kama alivyoahidi walipokuwa farashani. Pengine ulikuwa ujanja wa kumpeleka mgeni wake chumbani.
"Debbie. Hizo picha nzuri sana … akina nani hao?" Murphy aliuliza kwa kushtukiza.
Debbie aliziangalia picha alizokuwa akizisema Murphy halafu akamwangalia tena.
"Huyo wa kushoto ni shujaa wa maisha yangu. Frida Kahlo. Hiyo michoro mitatu unayoiona hapo ukutani ni miongoni mwa kazi zake maridadi. Maarufu dunia nzima. Alizaliwa Coyoacán na kufia Coyoacán. Ndiyo maana Coyoacán ni sawa na Maka kwangu; tumenunua hata 'managerie' hapo, shamba la wanyama wa mwitu ... Huyo wa katikati ni Marciano. Hapo ni miaka kumi iliyopita. Alikuwa bado mdogo, miaka kumi na tisa. Aliipiga katika sherehe yangu ya 'quinceañera' ya kutimiza miaka kumi na tano, kipindi hicho tukiwa bado tunaishi La Soledad, Canatlan, Durango; halafu akaniletea kama zawadi baada ya kuisafisha katika studio ya mji wa nyumbani kwao Ciénega de Caballos ... Huyo wa kulia ni rafiki yangu. Wanda Castellanos. Lakini kuanzia Jumanne iliyopita si rafiki yangu tena."
"Jumanne ya jana au ya wiki iliyopita?" Murphy aliuliza kwa shauku.
"Jumanne aliyokufa Marciano."
"Kwa nini?"
"Baba yake ndiye aliyeniingiza katika matatizo."
Kengele ililia katika kichwa cha John Murphy kwa mara nyingine. Lakini hakupenda kuwa na pupa. Hivyo, aliamua kubadili mada ili suala la Wanda walizungumze baadaye.